“Niiteni Raila Amolo Odinga”


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kulia) na Raila Odinga wakibadilishana mawazo 

Amesema anaona watu wakipata taabu sana kuhusu namna watakavyomuita kwa kuwa hayuko serikalini kwa sasa. Anasema yeye ana jina yale halisi, watumie hilo.

Nairobi. Kiongozi wa Muungano wa Mageuzi na Demokrasia (Cord), Raila Odinga, amewataka watu wasisumbuke bure jinsi watakavyomwita, kwa kuwa hahitaji ‘huruma za watu’.
Alisema kuwa ameyaweka nyuma yaliyoibuka kutokana na mvutano wa Uchaguzi Mkuu wa mwezi uliopita na kuwakosoa wale wenye utata kuhusu jinsi watakavyomwita mbele ya umma.

“Nimeketi hapa na kutazama jinsi kila mtu akitatizika atakavyoniita. Yeyote asisumbuke kusema mimi ni nani wa zamani. Mimi ni Raila Amolo Odinga,” alisema.

Odinga alikuwa akizungumza katika shule ya msingi ya Onjiko eneo Bunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu, wakati wa mazishi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Walimu nchini Kenya, (Knut) David Okuta.

Watu waliosimama kuzungumza kabla yake walitatizika kumtaja. Baadhi walimwita Waziri Mkuu mstaafu huku wengine wakimwitia ‘Aliyekuwa Waziri Mkuu’ na hata wapo waliomwita moja kwa moja ‘Waziri Mkuu’.
Wadhifa wa Waziri Mkuu uliondolewa na Katiba, ambayo iliuvumilia hadi Serikali ya mseto ilipovunjika rasmi Machi 9, Rais Uhuru Kenyatta alipoapishwa.

Hata Rais Kenyatta aliposimama kuhutubia alimtaja Odinga kuwa ‘Ndugu yangu Waziri Mkuu’.
Alipozungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Odinga alilazimika kutumia lugha yake ya asili kuwahakikishia wafuasi wake kuwa bado ana umuhimu katika siasa za Kenya.

“Jokanyanam antie pod adhi nyime. Ka oluth kuon otur ok omwon tedo dhi nyime.” (Watu wa ziwa, bado ninaendelea mbele. Kuvunjika kwa mwiko, si mwisho wa kupika ugali). Kisha alirejea msemo huo wa Kiswahili alipowahakikishia wafuasi wake kote nchini kwamba yeye hajaporomoka kisiasa kwa kuwa ataungana na rais mstaafu Mwai Kibaki kwa ajili ya maendeleo.

“Serikali si ya sehemu moja ya Kenya tu ni ya watu wote. Nawasihi Wakenya wote tushirikiane ili kuleta maendeleo katika maeneo yote,” Rais Kenyatta alisema.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alisifu falsafa ya marehemu Osiany katika kupigania maslahi ya walimu.
“Osiany alikuwa akitilia maanani mahitaji ya kitaifa katika kila alilotenda. Nilifurahi kufanya kazi naye,” alisema.

Odinga alimsifu marehemu kwa weledi wake katika kujadili mambo yaliyowahusu walimu na pia kwa msimamo thabiti aliokuwa nao wakati wa kuwatetea aliokuwa anawawakilisha.
Odinga pia alitoa changamoto kwa Serikali iwaajiri walimu 80,000 zaidi ili kuziba pengo lililopo kwa sasa.
Previous
Next Post »