HATIMAYE kesi ya kijana Emmanuel Didas (26), aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu anayeidai Serikali fidia ya zaidi ya Sh1 bilioni, sasa itaanza kusikilizwa rasmi baada ya kuvuka vikwazo vilivyowekwa na Serikali.
Serikali ilikuwa imeweka pingamizi kadhaa ikitaka kesi hiyo itupwe kwa sababu mbalimbali, lakini Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam, Profesa Ibrahim Juma akatupilia mbali pingamizi zote.
Kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi nje na ndani ya nchi, itatajwa Jumatatu ijayo mbele ya Jaji Profesa Juma ili mawakili wa pande zote mbili waweze kukubaliana tarehe rasmi ya kuanza kuisikiliza.
Wakili Carnelius Kariwa anayemtetea mwathirika huyo, alilithibitishia gazeti hili jana kuwa mchakato wa usikilizwaji kesi hiyo sasa utaanza Jumatatu baada ya kuvuka vikwazo vilivyowekwa na Serikali.
“Kwanza Serikali ilikuwa ikipinga hatua ya Sisti Marshay kumsimamia ndugu yake katika kesi hii, pili walikuwa wanasema imepitwa na wakati lakini vikwazo vyote vimetupwa,” alisema Kariwa.
Didas alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu baada ya kupata ajali, lakini akafanyiwa upasuaji wa kichwa na mgonjwa mwingine aliyepaswa kufanyiwa upasuaji wa kichwa akapasuliwa mguu.
Kwa sasa Didas ambaye alifanyiwa upasuaji huo Novemba 1,2007 na Madaktari Bingwa wa Kitengo cha Mifupa (MOI), amepooza upande wa kulia wa mwili wake.
EmoticonEmoticon