Mwanafunzi auawa,anyofolewa viungo


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro.

MWANAFUNZI wa darasa la sita Shule ya Msingi Kasumulu, Kata ya Ngana, wilayani Kyela, Kaselema Mpale (14) ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali, kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake sehemu ya mwili.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Lucia Kamnyonge alisema tukio hilo lilitokea Februari 8, mwaka huu saa 1:30 usiku, alipotumwa na baba yake kwenda nyumba ya jirani kuchukua mpunga ambao ungetumika kwa chakula usiku.
Kamnyonge alisema mtoto wake hakupatikanika hadi alipokutwa siku ya pili yake, akiwa amechinjwa na kunyofolewa baadhi ya sehemu zake za mwili ambazo ni pua, mdomo, jicho, kuondolewa sehemu zake za siri na kuchunwa ngozi ya kichwa karibu na utosi na mwili wake kutundikwa juu ya mti.
Aliendelea kuwa baada ya hali hiyo taarifa ilipelekwa ofisi ya serikali ya kijiji, uliitishwa mkutano wa wananchi wote na walitawanyika kuanza kumtafuta mtoto huyo bila ya mafanikio.
Baadaye, baba yake alimkuta juu ya mti akiwa ametundikwa kichwa chini miguu juu na viungo vyake hivyo vikiwa vimenyofolewa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ibungumbati lilipotokea tukio hilo, Adam Mkese alidai tukio hilo limewashtua na kwamba, mkutano wa kijiji ulioitishwa kwa dharura wananchi walimhusisha baba mzazi wa mtoto huyo na mauaji hayo.
Mkese alidai watu wa kijiji hicho walimhusisha kutokana na mazingira tata ya kifo chenyewe na maelezo ya kujichanganya aliyoyatoa.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Naomi Charles alidai kuna dalili za mzazi huyo kuhusishwa na mauaji hayo na kwamba, polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Baruti Mwakasala alidai kuwa hali katika kijiji hicho siyo nzuri na kushukuru polisi kwa hatua za haraka walizochukua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kukiri kumshikilia baba mzazi wa mtoto huyo kwa uchunguzi zaidi.
 
Previous
Next Post »